Dodoma, 15 Agosti 2026 — Watendaji Wakuu wa ofisi mbalimbali za serikali wametakiwa kutenga siku maalum kwa ajili ya mazoezi kwa wafanyakazi wao mahala pa kazi, ili kuwajengea afya bora na utimamu kazini.

Kauli hiyo imetolewa na mgeni rasmi wa bonanza la uzinduzi wa michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), Katibu Mkuu Ofisi ya Rais — Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Seleman Mkomi, aliyemwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Mpogole Kusiluka. Bonanza hilo limefanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlini, jijini Dodoma.

Mgeni rasmi amesisitiza kuwa mazoezi ya mara kwa mara mahala pa kazi ni sehemu ya kujenga nguvu kazi yenye afya, na kuwataka waajiri kuweka mazingira yanayowawezesha watumishi kushiriki michezo na mazoezi.

Bonanza hilo ni hatua ya kuelekea Michezo ya SHIMIWI 2026 yanayotarajiwa kufanyika mkoani Kilimanjaro kuanzia tarehe 19 Septemba hadi 7 Oktoba 2026.