Dodoma, 15 Agosti 2026 — Watendaji Wakuu wa Wizara na taasisi za umma wametakiwa kuweka msisitizo kwa watumishi wa umma kushiriki kwenye michezo mbalimbali, pamoja na mazoezi ya mara kwa mara.

Kauli hiyo imetolewa na mgeni rasmi, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais — Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Seleman Mkomi, aliyemwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Mpogole Kusiluka, katika bonanza la uzinduzi wa michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) lililofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlini, jijini Dodoma.

Bw. Mkomi amesema ushiriki wa watumishi wa umma kwenye mazoezi na michezo mbalimbali unasaidia kuwajengea afya njema wao ambao wanakwenda kutoa huduma kwa wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Awali aliungana na Mwenyekiti wa SHIMIWI, Bw. Daniel Mwalusamba, kwa kumshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa ruhusa kwa watumishi wa umma kushiriki kwenye michezo mbalimbali. Pia alipongeza SHIMIWI kwa kuandaa bonanza lililofana kwa kushirikisha wanamichezo kutoka sehemu mbalimbali.

“Naona fahari kwa kunipa heshima kubwa ya kumwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi katika bonanza hili la uzinduzi wa michezo, kwa kuwa ndiye mkuu wa utumishi wa umma Tanzania. Basi waajiri wanaofanya kazi kwa niaba yangu huko sehemu za kazi wawaruhusu wanamichezo kushiriki kwenye mashindano haya. Huko nyuma tuliwahi kutoa agizo wahakikishe wanatenga bajeti kila mwaka za kuwaruhusu watumishi wao kushiriki kwenye michezo hii ya SHIMIWI, na ninaimani wametenga na watawaruhusu,” amesema Bw. Mkomi.

Aidha, amewaelekeza Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa SHIMIWI kuwasilisha ripoti itakayoonyesha idadi ya Wizara na Taasisi ambazo zimeshiriki na zile ambazo hazijashiriki kwenye michezo hii ya SHIMIWI 2026 itakayofanyika mkoani Kilimanjaro kuanzia tarehe 19 Septemba hadi Oktoba 7.

Amesema michezo ni haki ya watumishi kitaifa na kimataifa, kwani watumishi ndio wanategemewa kiuchumi, kijamii na katika utoaji wa huduma mbalimbali.